11 Julai 2023 - 19:37
Safari ya kwanza ya Rais wa Iran barani Afrika baada ya miaka 11

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumanne ya leo ameondoka nchini kuelekea barani Afrika kwa ziara ya siku tatu ya kuzitembelea nchi za Kenya, Uganda na Zimbabwe.

Katika ziara yake hiyo, Rais wa Iran atafanya mazungumzo na viongozi wenzake, kuhudhuria vikao vya wajumbe wa ngazi za juu, kushiriki katika mikutano na waandishi wa habari na kutia saini hati kadhaa za ushirikiano.

Sayyid Ebrahim Raisi ambaye amefanya safari 15 za kigeni akiwa Rais wa Iran, anahesabiwa kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu kuzuru Afrika baada ya kipindi cha miaka 11. Tarehe 15 Machi mwaka huu wa 2023, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza utayarifu wa Tehran wa kupanua zaidi ushirikiano na nchi za Kiafrika katika kikao na washiriki wa mkutano wa kwanza wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na nchi za Afrika Magharibi.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na licha ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitilia mkazo suala la kuimarishwa uhusiano na nchi za Kiafrika kutokana na mambo yanayofanana na yanayozikutanisha pamoja pande hizo mbili katika nyanya za kisiasa na kiutamaduni.

Serikali ya Awamu ya 13 ya Iran inayoongozwa na Sayyid Ebrahim Raisi pia inatilia maanani suala la kupanua uhusiano na nchi za Kiafrika kwa mujibu wa sera yake ya nje ya kuwepo ushirikiano wa pande nyingi za kiuchumi. Kuhusiana na hilo, mnamo Agosti mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian alitembea nchi za Mali na Tanzania na kuzungumza na viongozi wa nchi hizo za Kiafrika kuhusu njia za kupanua ushirikiano. Kutokana na mtazamo huu wa Serikali ya Awamu ya 13, mpango wa kupanua zaidi mauzo ya nje ya bidhaa zisizo za mafuta na kuimarisha uhusiano wa kibiashara na nchi za Afrika umeshika kasi zaidi, na katika mwaka mmoja na nusu uliopita, jumbe rasmi zaidi ya hamsini kutoka Afrika zimefanya safari nchini Iran na kutia saini mikataba kadhaa ya maelewano.Japokuwa kiwango cha biashara kati ya Iran na nchi za Afrika kinaongezeka, lakini bado kiko mbali na lengo lililoainishwa la kufikia dola bilioni 10 kwa mwaka. Kwa sasa, uagizaji wa bidhaa kutoka nje wa nchi za Afrika umetangazwa kuwa karibu dola bilioni 600, lakini sehemu ya Iran katika biashara hiyo haifiki dola bilioni 2. Hii ni licha ya kwamba, kuna nyuga nyingi na pana za ushirikiano na kupanua uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Afrika, hususan katika nyanja za nishati, uhandisi, uchukuzi, kilimo na madini.

Alireza Peyman Pak, Katibu wa Baraza Kuu la Usimamizi la Chama cha Wafanyabiashara wa Iran, anasema katika suala hili kwamba: Uanzishwaji wa usafirishaji wa uhakika wa meli, ujenzi wa miundombinu na kusainiwa makubaliano ya kupunguza ushuru wa biashara, vinaweza kuwa na taathira kubwa katika kuzidisha biashara kati ya Iran na bara la Afrika."

Mbali na umuhimu wa kiuchumi wa uhusiano wa Iran na bara la Afrika, kustawishwa uhusiano na nchi za bara hilo katika masuala ya siasa na utamaduni pia kuna umuhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imewekewa vikwazo na mashinikizo ya kisiasa ya nchi za Magharibi. Nchi 50 kati ya 54 za bara la Afrika ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), baadhi zikiwa chini ya vikwazo; Pia kuna nchi 30 za Kiislamu katika bara hilo, na zaidi ya 50% ya wakazi wake ni Waislamu.Ni wazi kuwa uwekezaji na ushiriki wa kina wa Iran katika bara la Afrika sio tu kwamba una manufaa ya kiuchumi kwa pande zote mbili, bali pia utaongeza hadhi na taathira za kisiasa na kiutamaduni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika bara hilo. Kwa sababu hiyo, safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi tatu za Afrika yaani Kenya, Uganda na Zimbabwe inaweza kutoa bishara njema ya harakati mpya ya kupanua uhusiano na ushirikiano wa pande mbili hususan katika nyanja za kiuchumi na kibiashara.

342/